Mgosi aja na mikakati kabambe soka la wanawake
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Musa Hassan 'Mgosi' ameweka wazi kuwa msimu huu wamejipanga vema kuhakikisha wananyakua taji la ligi kama ilivyo kwa upande wa wanaume.
Kikosi hicho kimeanza mazoezi leo Jumanne Juni 9 na kesho kitaingia kambini tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi ya Wanawake utakaoanza Juni 22, mwaka huu.
Mgosi amesema kwenye mzunguko wa kwanza hawajapoteza hata mechi moja na watahakikisha wanaendeleza moto huo hadi wanachukua ubingwa.
"Mpango wetu msimu huu ni kuchukua ubingwa na hadi sasa tupo kileleni mwa msimamo. Kama ilivyo kwa timu ya wanaume na ile ya vijana dhamira ni moja tu kuchukua mataji yote tunayo shiriki msimu," amesema Mgosi.
Mgosi ameongeza kuwa wachezaji kutoka mikoani wako safarini kurejea jijini Dar es Salaam tayari kuingia kambini kesho kujiandaa na mikiki mikiki ya ligi.
"Hawa wachezaji unaowaona ni wa hapa mjini wale wa mikoani wapo njiani na kesho tutaingia kambini rasmi kujiandaa na ligi na mchezo wetu wa kwanza utakuwa dhidi Ruvuma Queens utakaofanyika Juni 22," amesema Mgosi.
Hadi ligi hiyo inasimama kupisha mlipuko wa virusi vya homa ya corona, Simba Queens inaongoza msimamo ikiwa na pointi 26 baada ya kucheza mechi 10 na kubaki 11.


No comments:
Post a Comment