BOBI WINE
Viongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye na Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine wameunda muungano wa upinzani.
Robert Kyagulanyi wa vugu vugu la People Power kwa pamoja na Dkt. Kizza Besigye ambaye chama chake FDC kinaongozwa na Amulati, Meya wa Kampala Erias Lukwago wa chama cha DP, Rais wa chama cha CP Keny Lukyamuzi, rais wa chama cha JEEMA Asumani Bsalirwa na wengine wengi wamezindua rasmi muungano mpya wa upinzani kuwa na mshika bendera mmoja katika uchaguzi ujao mwaka 2021 dhidi ya Rais Museveni.
Akizindua rasmi muungano huo katika wilaya ya Wakiso, Robert Kyagulanyi ameutaja muungano huo kwa jina la 'United forces of change' na kusema kuwa kufikiwa walipo, wamepiga hatua kubwa.

''Nataka kushukuru viongozi wetu walioona njia, wakafuata njia hiyo na kutuonyesha njia,'' Kyagulanyi amesema hayo.
Aidha ameweka wazi kwamba hakuna njia nyingine zaidi ya kuungana.
''Ni lazima tushirikiane kwa manufaa ya nchi yetu.'' Kyagulanyi ameongeza hayo huku akisisitiza kuwa njia walioshika ndio sahihi.
Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mbunge ameweka wazi kwamba wao (walioungana) sio maadui na kadiri wanavyoendelea kupigana vita wenyewe kwa wenyewe ndivyo wanavyoendelea kuchelewesha mabadilko ambayo raia wamekuwa wakisubiri kwa hamu.
Robert Kyagulanyi ameeleza kwamba kufikia wanacholenga kunaweza kufanikiwa tu kwa ushirikiano wa watu.
''Natoa wito kwa raia wote wa Uganda msilale badala yake mpaze sauti zetu,'' Kyagulanyi amesema na kusisitiza kwamba kampeni yao ni ya amani.
Katika hotuba yake, amemnukuu Malcolm X ambaye alikuwa mwanaharakati wa haki za kiraia za Waafrika-Waamerika ''Mikakati inaweza kutofautiana, hatua za kuchukua na mbinu zinaweza kutofautiana lakini lengo likawa moja.''
Viongozi wa vyama viwili vikuu vya upinzani vya Kizza Besigye na Robert Kyagulanyi wamekuwa wakikutana mara kadhaa kuandaa mikakati ya kuunda muungano huo wa "United force of change".
Wabunge wengine pamoja na wafuasi wao ni miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi huo.
Na wale waliokuwepo walifuata kanuni ya kutokaribiana ili kuzuia usambaaji wa virusi vya corona.
Hata hivyo mkutano huo umesambaratishwa na polisi dakika za mwisho.



No comments:
Post a Comment