
Hii ikiwa ni kashfa ya hivi punde kando na nyingine ambazo zimeshuhudiwa katika kpindi cha siku za nyuma ambazo hadi hii leo hazijatatuliwa.
Wakenya wamejitosa katika mitandao ya kijamii kuelezea hasira na kuchoshwa kwa kile wanachotaja kuwa ni vitisho vya bure kwa viongozi wafisadi katika serikali
Baadhi wamekuwa wakieleza kwamba wanahisi Rais hajachukua hatua stahiki na kwa muda mrefu kufikia sasa amewaendekeza 'wahalifu' katika serikali.
Kwa kutumia #MrPresidentTumechoka raia wameelezea kuchoshwa kwao na matukio ya ufisadi Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe amekiri hivi karibuni kwamba umma unazidi kuudhika kutokana na kukithiri kwa visa hivyo vya rushwa.
Ni nani wa kuwajibika?
Rais Uhuru Kenyatta ameeleza kwamba watuhumiwa wa ufisadi watachukuliwa hatua.
'Tuungane pamoja na tuseme ya kwamba tutapambana na tutapiga vita ufisadi tukiwa kitu kimoja.
Kwasababu hatuna njia nyingine, Wakenya wanahitaji barabara mahosiptali, stima, vijana wetu wanataka kazi, mambo haya hatutayapata tukifuata mwenendo ambao upo hivi sasa - 'Get rich quick' - hiyo haiwezi kutufikisha mahali ambapo taifa tunataka kwenda' ameeleza rais Uhuru Kenyatta hivi maajuzi akizungumza katika mazishi aliyoyahudhuria huko Muranga Kenya ya kati.
Mnamo 2015, rais Uhuru alitangaza rasmi vita dhidi ya ufisadi kama tishio kwa usalama wa taifa ambalo lilikuwa likipindukia.
Tangu hapo, kiongozi huyo amekuwa akisisitiza tishio la kuchukua hatua dhidi ya maafisa wanaotuhumiwa katika kashfa za rushwa.

Licha ya kusimamishwa kazi kwa baadhi ya mafisa serikalini, na wengine kushtakiwa, bado kashfa za ufisadi zimekuwa zikiibuka nchini.

Jinamizi la Rushwa limemshinda nguvu rais Kenyatta?
Katika orodha ya mataifa yanayoshuhudia ufisadi Kenya ipo katika nafasi ya 144 chini ya mataifa 180 kwa mujibu wa utafiti wa shirika la kimataifa la Transaparency International mnamo 2018.
Kwa miaka mingi, kumekuwa na wito wa kwamba ufisadi unastahili kutangazwa janga la kitaifa nchini Kenya.
Ufisadi una historia kubwa nchini kutokana na kudhihirika katika serikali za viongozi tofuati tangu Kenya kujinyakulia uhuru.
Wakenya wameanzisha mjadala na kulizungumzia donda sugu la rushwa Kenya katika mitandao ya kijamii.
Kwa kutumia #MrPresidentTumechoka Baadhi wamezungumzia hasira walio nayo kwa wanachotajwa kuwa ni kupuuzwa kwa rushwa nchini na ahadi za bure pasi hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa katika serikali.
Baadhi hata wakikejeli uzito wa tatizo la rushwa Kenya:
Wengine wakilalamika kwamba Wakenya hawana namna ila kukaa na kutazama tu siku nenda siku rudi, na kulazimika kuzisikiza ahadi za bure.
Hatahivyo kuna wanaokiri kwamba jinamizi hilo la rushwa nchini sio jukumu la mtu mmoja, na kwamba kila Mkenya ana wajibu katika kulitatua suala hilo.
Licha ya kukamatwa na kushtakiwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa wizi wa pesa za umma nchini Kenya, baadhi ya raia wanasema hawana imani kuwa wahusika watakabiliana na mkono wa sheria , kutokana na kwamba washukiwa katika sakata za ufisadi zilizofichuliwa vipindi vilivyopita waliachiliwa.
Serikali ya rais Uhuru Kenyatta imekumbwa na sakata kadhaa katika siku za hivi karibuni katika kile kinachoonekana kushindwa kwa juhudi za kupambana na ufisadi.
No comments:
Post a Comment